Mapacha Wafa Maji, Mama Ajitupa Baharini Siku ya Eid
MAPACHA wawili waliokuwa wakiishi kata ya Kashai katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera walikufa maji juzi kwenye ufukwe za Ziwa Victoria wakati wakiogelea kusherehekea Eid, katika siku ambayo mama mmoja alijitupa baharini kutoka kwenye pantoni Feri, jijini Dar es Salaam kwa wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Agustino Ollomi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kamanda Ulomi alisema juzi majira ya saa 11:30 jioni, mapacha hao walikuwa wakiogelea ziwani katika eneo la Kiloyela lililopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani humo.
Marehemu mapacha hao walitajwa kuwa ni Hussein Hamis (12) na Hassan Hamis(12), na kwamba walikuwa wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kashai.
“Watoto hao walikuwa wa askari mwenzetu(wa) kitengo cha Usalama Barabarani," alisema Kamanda Ollomi na kwamba "walikuwa wakisoma darasa la saba.”
Alisema sababu ya kifo cha marehemu hao ni kuzidiwa na nguvu ya maji na kupelekea kuzama ambapo waliopolewa wakiwa wamefariki.
"Watoto wenzao baada ya kuona wenzao wakiendelea kuzama walipiga kelele ili kuomba msaada, lakini jitihada za kuwaokoa wakiwa hai zilishindikana," alisema.
"Tayari watoto hawa wamezikwa Juni 27 mwaka huu (jana) katika makaburi ya Kishenge, yaliyoko katika Manispaa ya Bukoba.
“Tunaendelea kuwasihi wazazi, kuendelea kuangalia usalama wa watoto wao hasa katika siku za sikukuu ili kuepusha madhara kama haya."
Jijini Dar es Salaam, mwanamke aitwaye Asha Yahya(30), mkazi wa Zanzibar anadaiwa kujirusha baharini akiwa katika kivuko cha MV Magogoni kwa lengo la kujiua, lakini wananchi waliwahi kumuokoa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Temeke, Andrew Satta alisema tukio hilo lilitokea majira ya 2:10 asubuhi wakati akitokea Kigamboni kuelekea Ilala na kwamba sababu za kutaka kujiua ni wivu wa kimapenzi.
"Baada ya kumhoji alituambia kwamba sababu ya kutaka kujiua, eti mume wake anataka kuoa mwanamke mwingine," alisema Satta.
Katika tukio jingine katika kipindi cha sikukuu, Jeshi la Polisi jana liliokota mwili wa mtumishi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Masoud Abdulrahman(27) katika ufukwe wa Kisiwa cha Mbutu, kilichopo Kigamboni.
Kamanda Satta alisema marehemu kabla ya kukutwa na umauti huo alikuwa na wafanyakazi wenzake 20 ambao walikwenda katika ufukwe huo kwa ajili ya kufurahia sikukuu ya Eid, lakini wakati wakiogelea wimbi kubwa la maji liliwapiga na hivyo wote kupotea.
Alisema hata hivyo, baada ya Jeshi la Polisi kufanya msako baada ya kugundua kwamba kuna watu waliosombwa na maji, waliwapata wenzake 20 ambao waliokolewa na kukimbizwa hospitali.
Kwa upande wa mkoa wa kipolisi wa Ilala, mtu mmoja ambaye jina lake halikujulikana mara moja aligongwa na basi la mwendokasi katika Barabara ya Uhuru na kufariki papohapo juzi pia.
Kamanda wa Polisi wa Ilala, Salum Hamdani, alisema mtu huyo aligongwa na gari hilo baada ya kuingilia barabara ya mwendokasi na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mapacha Wafa Maji, Mama Ajitupa Baharini Siku ya Eid
Reviewed by Unknown
on
05:35:00
Rating:
Hakuna maoni: