SERIKALI YATOA KAULI HII KUHUSU WATANZANIA WATAKAOTIMULIWA NA TRUMP MAREKANI

Serikali imesema kuna Watanzania wengi wanaoishi Marekani kinyume cha sheria, lakini haijui idadi yao wakati Rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump akisubiriwa kutekeleza ahadi yake ya kutimua wahamiaji haramu.
Kuchaguliwa kwa Trump kuwa Rais wa 45 wa Taifa hilo kubwa, kumeibua hofu miongoni mwa kwa mataifa mbalimbali kuhusu raia wao wanaoishi bila ya nyaraka halali kutokana na sera za mfanyabiashara huyo maarufu za kutotaka wageni haramu.
Awali, Serikali ya Rais Barack Obama ilitoa ahueni kwa watu wanaosadikiwa kuwa milioni 11.1 (kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014 za taasisi ya utafiti ya Pew ya Marekani) baada ya kuwaruhusu kupitia mchakato ambao ungewapa uhalali wa kuishi nchini humo.
Lakini katika kampeni zake, Trump alisema hahitaji wageni walioingia Marekani kwa kukwepa sheria na hivyo atawatimua ili wakaanze mchakato wa kuomba kuingia Marekani wakiwa kwenye nchi zao.
Akizungumza na Mwananchi juzi, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje, Robi Bwiru alisema: “Kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi Marekani lakini kwa kuwa suala la mtu kutaka kutambulika na ubalozi wake ni la hiari, hatuna idadi kamili ya Watanzania ambao wapo kule bila nyaraka halali.”

Kuhusu misimamo ya kiongozi huyo kutoka chama cha Republican dhidi ya nchi za Afrika, Bwiru alisema Tanzania haiwezi kutoa msimamo wowote kabla ya kuona utekelezaji wa ahadi zake.

Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya Pew, Wamexico ndiyo wanaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wageni wanaoishi bila ya nyaraka halali wakiwa asilimia 52, lakini kutokana na uchumi wa Mexico kuimarika pamoja na ulinzi mkali mpakani, idadi yao inapungua.

Badala yake, watu kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwamo Tanzania, wameongezeka katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Pew inakisia kuwa idadi ya wageni kutoka Afrika wanaoingia isivyo halali imeongezeka hadi kufikia asilimia 37.5, wakati kutoka barani Asia imeongezeka hadi asilimia 11.5 na kutoka Amerika ya Kati ni asilimia 6.3.

Pew inaeleza kuwa sababu za kuongezeka kwa wahamiaji haramu ni vurugu Afrika ya Kati na ukosefu wa ajira barani Asia na Afrika.

Katika kampeni zake, Trump alisema atatekeleza msimamo wake wa kuwarejesha wahamiaji haramu, ikiwa ni pamoja na kujenga ukuta kwenye mpaka wa nchi hiyo na Mexico.

“Nitaanzisha kikosi maalumu cha kuwafukuza wahamiaji nchini. Kazi yake kuu itakuwa ni kuwasaka na kuwarejesha walipotoka wahamiaji haramu walioingia Marekani kwa kukwepa sheria za nchi, kama alivyozikwepa Hillary Clinton, pengine naye watamfukuza,” alisema Trump.

Aliongeza kuwa ujumbe wake kwa ulimwengu mzima ni kwamba haiwezekani kupata uraia wa Marekani kwa kuingia nchini humo kinyume na sheria
SERIKALI YATOA KAULI HII KUHUSU WATANZANIA WATAKAOTIMULIWA NA TRUMP MAREKANI SERIKALI YATOA KAULI HII KUHUSU WATANZANIA WATAKAOTIMULIWA NA TRUMP MAREKANI Reviewed by Unknown on 05:55:00 Rating: 5

Hakuna maoni:

Facebook

klin zepp. Inaendeshwa na Blogger.