DKT JOHN POMBE MAGUFULI MCHUNGAJI NG'OMBE NZURI TU ALIYEIBULIWA KIPAJI CHA SIASA NA WAZEE KIJIJI CHA RUBAMBANGWE.



Waziri wa Ujenzi ,Dk.John Pombe Magufuli. 


Asili ya Kijiji cha Rubambangwe kilichopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita ni eneo lililotumiwa na wawindaji baada ya shughuli zao kwa ajili ya kuwamba ngozi za wanyama mbalimbali. 


Kwa tafsiri ya wakazi wa eneo hili kwa msaada wa mkalimani, ‘Rubambangwe’ ni neno linalomaanisha ‘mwambaji wa chui’ pia ni miongoni mwa wanyama wakali waliowindwa na ngozi zao kuwambwa eneo hili. 


Barabara ya lami inayotoka Bukoba kuelekea Mwanza inakatiza katikati ya eneo hili. Hivi sasa eneo hili limezungukwa na majumba ya kisasa na si pori lililokuwa maficho ya wanyama na eneo la kukaushia ngozi. 


Hapa ndipo amezaliwa na kukulia Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Chato. Hapa ndipo unapoweza kukutana na baadhi ya wananchi ambao wanafahamu maisha yake ya ujana na hatua alizopita hadi kufika alipo. 


Kuna simulizi za kusisimua kuhusu maisha ya John Magufuli ambaye wananchi wengi wa Jimbo hili wanamtumia kama alama ya ushindi akihusishwa na mafanikio ya kujitenga kutoka Wilaya ya Biharamulo hadi wakapata jimbo na Wilaya. 


Ujio wa wilaya mpya ya Chato umesababisha jina la Rubambangwe kutoweka na badala yake kuzaliwa kwa kijiji kipya cha Mlimani ambacho sehemu kubwa ya majengo ya halmashauri yapo eneo hili. 


Pia kwa mujibu wa maelezo ya wenyeji ambao wengi ni wahamiaji, maana ya jina Chato ni nyoka aina ya chatu ambao walikuwa wakipatikana maeneo mengi kwenye ukanda huu wa kijani ambao uko kando ya Ziwa Victoria. 


Wananchi wamwachisha kazi 
Wananchi wanaamini kuwa kijana wao John Magufuli hakuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa mpaka aliposhawishiwa na wazee kugombea ubunge baada ya kuona wananchi wa ukanda huo wamekuwa wanyonge kwa muda mrefu. 


Mzee Emmanuel Francis anayakumbuka maisha ya ujana ya John Magufuli na kumuona kama mwanasiasa aliyeibuka kutokana na wazee kumuomba agombee ubunge wa Biharamulo. 


‘’Wazee tulikaa na kumuona huyu ndiye msomi wa kiwango cha juu anayeweza kutukomboa. Tulikuwa tunamfuatilia tangu akiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Sengerema hata alipokuwa mkemia wa Shirika la Pamba,’’ alibainisha Mzee Francis. 


Anasema John Magufuli hakuwakatisha tamaa na badala yake aliamua kujitosa kugombea na Phares Kabuye na baada ya matokeo anasema kuna mambo mengi yaliwashangaza wananchi wa kijiji hicho na maeneo mengine.


Tukio la John Magufuli kumshika na kumpongeza mshindani wake anasema liliwashangaza sana na kumuona kama kijana asiye na kinyongo jambo lililowashawishi kumuandaa kwa uchaguzi mwingine uliofuata. 


Hata hivyo, uvaaji wake wa miwani inasemekana ulimpunguzia kiasi fulani cha kura baada ya baadhi yao kuamini kuwa miwani hiyo ni kielelezo cha usomi na hivyo asingekuwa kiongozi wa kukimbiliwa. 


“Wasukuma tuna kasumba ya kupenda kupigiwa magoti, hivyo baadhi ya wananchi walipomuona ni kijana anayependa kuvaa miwani, walisema huyu ndiye atatusahau kabisa (kwamba hataweza kuwapigia magoti). Inawezekana kura zilipungua kwa hofu ambayo haikuwa na msingi,’’ anabainisha Mzee Francis. 


Pia anakumbuka kampeni za kwanza za John Magufuli zilivyotawaliwa na mbwembwe ambazo zilihusisha watu wa kambi yake kufunga kufuli ndogo kwenye mashati na suruali zao kama njia ya kumtangaza. 


Katika uchaguzi uliofuata Magufuli aliungwa mkono kwa kumshinda mpinzani wake Phares Kabuye na wananchi wanaamini huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuzaliwa upya kwa Jimbo la Chato na wilaya yake. 


Wananchi wanatumia kielelezo cha ongezeko la shule za sekondari na huduma mbalimbali kama matunda ya ukanda huo kujitegemea baada ya Magufuli kupata ubunge ambao anaushikilia hadi leo. 


Wananchi hao walisema kabla ya kujitenga, ukanda wa Chato haukuwa na shule yoyote ya sekondari na wanafunzi walilazimika kwenda kusoma Shule ya Sekondari ya Katoke wilayani Biharamulo. 


Leo wanajivunia kuwa na shule nyingi za sekondari kama ya Muungano, Meghji na Chato na nyingine zikiwa na kidato cha tano na sita, suala ambalo Mzee Francis anaamini lisingewezekana bila ujio wa Magufuli. 


Katika ngazi ya uongozi wa Serikali za Mitaa, Malele Matonange, kiongozi wa karibu katika kitongoji cha Mwenge yalipo makazi ya Magufuli, anasema anapata ushirikiano kutoka kwa waziri huyo. 


Anamfahamu Magufuli kama kijana aliyekulia kijijini hapo kabla ya kuibuliwa na wazee waliomfuata na kumshawishi agombee ubunge kwa kuwa kwa wakati huo ndiye msomi aliyeonekana anaweza kuwakomboa. 


Alikuwa mchunga ng’ombe 
Familia ya Pombe Magufuli ilikuwa ya wafungaji, hivyo watoto waliozaliwa katika kaya yake wasingeweza kulikwepa jukumu la kuchunga ng’ombe malishoni kama ilivyo katika maeneo mengi nchini.


Hata wakati wa likizo, wananchi walikuwa wakimuona John akifanya kazi za kawaida za nyumbani ikiwa ni pamoja na kuchunga ng’ombe na kukamua maziwa na mara kadhaa wakati wa likizo alizungukia wananchi kijijini kuwasalimia. 


“Baba yake alikuwa na mifugo mingi, lakini John hakuwa mtu wa kujikweza. Wakati wa likizo tulizoea kumuona akifanya kazi za nyumbani hata kwenda shambani kulima na kukamua maziwa baada ya ng’ombe kutoka malishoni,” anaeleza Mzee Francis. 


Wananchi wengine wanamueleza John Magufuli kama kijana ambaye hakuwa na majivuno pamoja na kuonekana msomi na wakati wa likizo hakuona aibu ya kushika jembe na kwenda shambani. 


Mwananchi mwingine, Maritha Rufunga ana kumbukumbu tofauti kuhusu maisha ya ujana wa Magufuli na hata hajasahau wakati mbunge huyo alipoanza safari yake kielimu kwa kujikwaa. 


“Hakuwa na majivuno na hata alipomaliza shule na kutochaguliwa baba yake alikataa asiendelee na masomo, lakini kuna mwalimu wake alikwenda kumuombea kwa baba yake ili akarudie shule,’’ alisema Maritha Rufunga. 


Anasema tangu wakati huo aliendelea na masomo na kufanikiwa kufika kiwango cha juu hata kuwa kiongozi wa kutegemewa na wananchi na kusema kuna mambo mengi yamebadilika wakati wa uongozi wake. 


Mtu mwingine, James Mchelle anayeishi karibu na yalipo makazi ya Magufuli, anasema walisoma wote Shule ya Msingi ya Chato na walikuwa marafiki. 


Anasema hata leo John Magufuli anapofika kijijini hakosi nafasi ya kuwatembelea jirani zake na wanakijiji wengine na hata kuhudhuria matukio mbalimbali ya kijamii, suala alilosema linamuweka karibu zaidi na wananchi. 


Magufuli na urais 
Miongoni mwa wakazi wa kijiji hiki, Emmanuel Francis anasema hana wasiwasi na Magufuli kama anatosha kuwa Rais wa Taifa hili kwa sababu ana uzoefu mkubwa kiuongozi kutokana na wizara alizoongoza katika awamu tofauti. 


‘’Amepita wizara nyingi bila kuwa na tuhuma za ubadhilifu kama ilivyotokea kwa mawaziri wengine. Alionyesha uadilifu na kila wizara aliyoongoza ilionekana kuwa imara na yenye mafanikio,’’ anasema Francis. 


Anabainisha kuwa Magufuli akichukua fomu ya kugombea nafasi ya urais, atamuunga mkono na anaamini kuwa anaweza kuungwa mkono na wananchi wengi kutokana na historia yake ya kuwatumikia kwa uadilifu.Hata hivyo, wasiwasi wake ni kuwa anaamini waadilifu wa aina yake ni vigumu kupata nafasi hadi kufikia kiwango cha kupendekezwa kuwania uongozi wa nchi kwa kile alichosema kuna makundi hayawapendi watu kama Magufuli.MWANANCHI
DKT JOHN POMBE MAGUFULI MCHUNGAJI NG'OMBE NZURI TU ALIYEIBULIWA KIPAJI CHA SIASA NA WAZEE KIJIJI CHA RUBAMBANGWE. DKT JOHN POMBE MAGUFULI MCHUNGAJI NG'OMBE NZURI TU ALIYEIBULIWA KIPAJI CHA SIASA NA WAZEE KIJIJI CHA RUBAMBANGWE. Reviewed by Unknown on 10:58:00 Rating: 5

Hakuna maoni:

Facebook

klin zepp. Inaendeshwa na Blogger.